Kwa mujibu wa idara ya kimataifa ya Shirika la Habari la Hawza, katika kukaribia kumbukumbu ya kwanza ya Shahidi Sayyid Hassan Nasrallah, katibu mkuu wa zamani wa Hizbullah na Sayyid wa Mashahidi wa Muqawama ndani na nje ya Lebanon, tunashuhudia kuhuishwa kwa kumbukumbu na utambulisho wa vipengele vya shakhsia na mwenendo wa maisha ya Sayyid wa Muqawama.
Miongoni mwa sifa mashuhuri za Shahidi Sayyid Hassan Nasrallah ni ukaribu wake wa kipekee na Iran na Wairani pamoja na uongozi wa Iran kuanzia zama za Imam Khomeini (r.a) na Kiongozi wa Mapinduzi wa Irani wa sasa akiwa mwakilishi wa Imam (r.a) nchini Lebanon hadi kipindi cha uongozi wake.
Kitabu Ruh al-Amin kilichoandikwa na Elaheh Akhareti kimekusanya, kutafsiri na kuhuisha sehemu za hotuba na mahojiano ya Sayyid wa Muqawama.
Katika sehemu za kitabu hiki, Sayyid wa Muqawama katika mahojiano yake alieleza uhusiano wake na uongozi wa Iran, ndugu zake Wairani, na pia akasimulia kumbukumbu za kipindi alipochaguliwa kuwa Katibu Mkuu na uhusiano wake wa karibu na wa kirafiki na Sayyid Abbas Mousavi, Katibu Mkuu wa kwanza wa Hizbullah.
Sayyid Hassan Nasrallah katika mazungumzo yake ameeleza hatua za awali za kuundwa kwa Hizbullah na kwamba tangia mwanzo yeye na wajumbe wengine wa Hizbullah walikuwa wakinufaika na tajiriba za ndugu zao Wairani, kuhusu safari za kwenda Iran alisema:
“Kila mwaka ndugu zetu walikuwa wakienda Iran mara mbili au tatu, yaani karibu kila baada ya miezi sita walikuwa na safari ya kwenda Iran ili kupata taarifa za hali ya Iran na mitazamo ya viongozi wa Iran kuhusu mabadiliko ya eneo, wakati huo matukio ya kikanda yalikuwa yakitokea kwa kasi kubwa na ndugu zetu walihitaji ushauri wa mara kwa mara na Iran pamoja na msaada wao. Mara nyingi likijitokeza jambo muhimu au la dharura, walinituma mimi Iran kwa sababu wakati huo nilikuwa mdogo zaidi miongoni mwao na kwa kuwa sikujulikana sana, sikukabiliwa na tishio kubwa la kiusalama na safari zangu hazikuwa na ugumu.
Zaidi ya hayo nilikuwa na ujuzi zaidi wa lugha ya Kifarsi kuliko ndugu zangu wengine, hivyo walipendelea niende Iran. Tangu mwanzo kulikuwepo mapenzi na upendo kati yangu na ndugu Wairani, Marafiki walikuwa wakiniambia: wewe unawapenda Wairani na Wairani pia wanakupenda wewe, basi nenda mwenyewe Iran ukafanye jambo fulani...”
Mikutano ya karibu ya Sayyid wa Muqawama na Kiongozi (Ayatullah Khamenei)
“Nilikuwa nikiwasilisha ujumbe wa ndugu zangu kwa Mtukufu Kiongozi, na mara nyingi nilikaa naye kwa saa moja au mawili, nilipokuwa nikimaliza na kujiandaa kuondoka, yeye alikuwa akiniambia: kwa nini unaharakisha? Kaa hapa na kama bado kuna jambo ulisemee. Nilihisi sitaki kuchukua muda wake, lakini yeye alikuwa na subira kubwa.”
Ahadi ya Imam Khomeini (r.a) kwa Sayyid wa Muqawama
“Mwaka 1989, takriban mwezi mmoja au miwili kabla ya kufariki kwa Imam (r.a), nikiwa mjumbe wa Baraza la Uongozi la Hizbullah na mkuu wa masuala ya kiutendaji wa jumla wa Hizbullah, nilisafiri Iran. Katika safari hiyo nilieleza kuwa ningependa kupata fursa ya kumuona Imam. Nikaambiwa kuwa Imam yuko kitandani anaumwa na hatoi nafasi ya kukutana na mtu yeyote. Hata hivyo, nikasema nitajitahidi. Wakati huo mmoja wa marafiki zetu katika nyumba ya Imam, Sheikh Rahimian, alikuwa akiwajali sana Wana-Lebanon. Alizungumza jambo hilo na Sayyid Ahmad. Siku ya pili ya safari yangu nilijulishwa niwe tayari kwa ajili ya kukutana.
Siku iliyowadia, niliingia kumuona Imam. Hakukuwa na mtu yeyote pale, wala maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje au wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi waliokuwa kawaida wakihudhuria. Sheikh Rahimian baada ya kuniingiza hadi chumba cha Imam, aliniacha peke yangu. Nilipatwa na hali ya woga kutokana na ukubwa wa hadhi ya Imam. Imam alikuwa amekaa kwenye sofa na mimi nikaketi chini. Nilipigwa na butwaa kiasi kwamba sauti haikutoka. Imam akaniambia: “Kaa karibu zaidi.” Kisha akajibu maswali yangu kuhusu hali ya wakati ule Lebanon. Baada ya hayo akatabasamu na kusema: “Waambie ndugu zetu wote kwamba tutabakia daima pamoja nanyi.” Huu ulikuwa mkutano wangu wa mwisho na Imam.”
Baada ya kufariki Imam (r.a), Baraza la Hizbullah lilihisi wasiwasi kuhusu hali ya baada ya kiongozi mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu wa Iran, wasijue nani atakayekuwa kiongozi mpya. Sayyid Hassan Nasrallah katika sehemu ya kumbukumbu zake alisema:
“Kutangazwa kwa mrithi wa Imam (r.a) kuliondoa wasiwasi wote, hofu na mashaka kuhusu mustakbali. Utulivu wa ajabu ulitanda katika nyoyo zetu.”
Maoni yako